Seliphar, Kakamega
Kila siku, kila uchao visa vya dhuluma dhidi ya watoto vinaongezeka katika kaunti ya Kakamega. Ni kipi kinachosababisha visa hizi? Ni hatua gani inayochukuliwa dhidi ya wale wanaotenda unyama huu? Haya ni baadhi tu ya maswali ambayo kupata majibu yake ni muhali.
Hata hivyo wanaskauti kutoka katika kaunti ya Kakamega wamejitosa uwanjani kukashifu maovu hayo dhidi ya watoto. Wanaskauti hao wameshiriki matembezi ya amani ya kuwahamasisha wakaazi kuwa mstari wa mbele katika kuripoti visa hivyo punde tu vinapototekea katika jamii.
Matembezi hayo yaling’oa nanga katika eneo bunge la shinyalu ambapo yalihusisha wanafunzi wa shule za msingi wakieneza ujumbe kwa umma wa kukomesha dhuluma dhidi ya watoto.
Sharon Ingato aliyeongoza kikosi hiki alisema kwamba dhuluma dhidi ya watoto zina madhara mengi kama vile kususia masomo, mimba za mapema na hata sehemu za mwili kuharibika kwa mfano watoto wa kiume wanapo lawitiwa .
‘Naomba serikali iweke sheria kali kwa watu watakao patikana kwa makosa yanayohusiana na watoto , pia watoto muwe makini sana mnaporipoti visa hivi maana si kila mtu atakusaidia kupata haki.’ Florence Awino adokeza
‘Kila mtoto ana ndoto yake maishani, tunapowadhulumu hawa watoto tunaua ndoto zao maana kuna wale baada ya kitendo hicho hawatarudi shuleni , kuna mwingine atajitoa uhai. Tumejitokeza ili tupiganie haki za watoto na tukomeshe dhuluma dhidi ya watoto katika kaunti hii.’ Sharon alieleza.
Matembezi haya yaliungwa mkono na baadhi ya walimu katika eneo hilo na kuwasihi watoto kuwa makini wanaporipoti visa kama hivi maana si kila mtu ni mwaminifu na si wote watahakikisha kwamba haki inapatikana.
‘Naomba serikali iweke sheria kali kwa watu watakao patikana kwa makosa yanayohusiana na watoto , pia watoto muwe makini sana mnaporipoti visa hivi maana si kila mtu atakusaidia kupata haki.’ Florence Awino adokeza
Viongozi wa wanaskauti wameionya jamii dhidi ya kushiriki mazungumzo na kutatua visa vya dhuluma nyumbani, wakisema kuwa kwa mara nyingi wahasiriwa hunyimwa haki
‘’Wale wanaotekeleza maovu haya wachukuliwe hatua kali ndiposa idadi ya vitendi hivi iweze kurudi chini. Tunaomba jamii iwache sheria ichukue mkondo wake, wasiingile kati kwa kutaka kesi hizi zisuluhishwe nyumbani hii ndio sababu kubwa ya kuongezeka kwa dhuluma dhidi ya watoto.’’ Sharon alionya.
Mwisho